Poems

Fasihi

Maneno yangu kumeza tena sasa siwezi.

Lakini kuonyesha ukweli na kuutafuta
Nitaendelea: mimi ni kama boga.
Nimepandwa katikati, bustanini,
Na kama boga nitatambaa chini
Zote pande, kuikwea miti ya hekima
Na yote magugu koo kuyakaba.
Bila woga, bila nyuma kurudi nitashambulia
Ya binadamu matendo bado yakihema.
            Halafu wakati
            Ujao utafika
            Matunda nitatoa
            Makubwa madogo
            Mazuri mabaya
Wakati utafika watakapokuja wajuzi
Kwa jembe la wino kunipalia.
Wala mboga za majani watanichuma.
Utafika, wa maboga kuwa mikata.
Machafu na safi yatachotwa
Na nitaingia mitungi ya kila mji-shamba.
Watoto mikononi mwao watanichezea.
Chini wataniangusha na kunipasua.
Lakini mbegu, mbegu zitabaki.
            Mimi ninajua
            Hatari sina
            Wajibu msomaji
            Mjini na shamba
            Vizuri kunichambua.
 
Halafu utafika ule wakati
Watumia vikombe dhahabu na glasi
Pembeni kwa chuki kunitupa,
Na nitakuwa nyuma ya wakati
Lakini wakisahau wahenga
Kata na mboga walitumia
Msingi wa wao utamaduni
Watakuwa wameutupa.
Kumbukeni, kumbukeni, kumbukeni.