Poems

Kizuizini

Nikiwa na njaa na matambara mwilini
          nimehudumika kama hayawani
Kupigwa na kutukanwa
          kimya kama kupita kwa shetani.
Nafasi ya kupumzika hakuna
          ya kulala hakuna
          ya kuwaza hakuna.
Basi kwani hili kufanyika.
Ni kosa gani lilotendeka
Liloniletea adhabu hii isomalizika?
 
Ewe mwewe urukae juu mbinguni
          wajua lililomo mwangu moyoni.
Niambie: pale mipunga inapopepea
           ikitema miale ya jua
Mamaangu bado angali amesimama akinisubiri?
Je nadhari yake hujitokeza usoni
           ikielekea huku kizuizini?
 
Mpenzi mama, nitarudi nyumbani
Nitarudi kama hata ni kifoni
Hata kama maiti yangu imekatikakatika
           vipande elfu, elfu kumi
           Nitarudi nyumbani
Nikipenya kwenye ukuta huu
nikipitia mwingine kama shetani,
Nitarudi mpenzi mama ....
                                      hata kama ni kifoni.